Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepiga marufuku matumizi ya viberiti,
mishumaa na heater za kuchemshia maji kwa wanafunzi wa bweni ili
kuepusha majanga ya moto na atakayekutwa atachukuliwa hatua kali.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitembelea Shule ya Sekondari Lindi baada ya shule hiyo kuteketea kwa moto hivi karibuni.
“Kuna tabia ya baadhi ya wanafunzi hasa wa masomo ya fizikia kutengeneza
vifaa vya kienyeji vya kuchemsha maji mabwenini jambo hili ni la hatari
kwani linaweza kusababisha ajali ya moto, hivyo ni marukufu kwa
mwanafunzi kutumia vifaa hivyo,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Julai 17, 2016) katika
harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari
Lindi yaliyoungua moto usiku wa kuamkia Julai 10 mwaka huu.
Katika ajali hiyo shule imeathirika kwa asilimia 34 ambapo vyumba tisa
vya madarasa, jengo lenye matundu 26 ya vyoo na jengo la maabara ya
kemia na fizikia yameungua na kusababishia hasara ya sh. milioni 682.78.
Waziri Mkuu amesema kwa namna ambavyo majengo hayo yameungua ni vema
yakavunjwa na kujengwa upya ambapo aliwataka kutumia nafasi hiyo kwa
kujenga jengo la ghorofa ili kutumia eneo dogo kwa kujenga madarasa
mengi.
Pia alimuagiza Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kuhakikisha fedha
zitakazopatikana katika harambee hiyo zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Harambee ilihudhuriwa na mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa, mke wa Rais
mstaafu wa awamu ya nne, mama Salma Kikwete, mkuu wa mkoa wa Mtwara,
Halima Dendego pamoja na wadau wa maendeleo na wanafunzi waliosoma shule
hiyo akiwemo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amezitaka taasisi mbalimbali nchini
kufunga vifaa vya kuzimia moto katika majengo yao kwa ajili ya kuvitumia
pindi ajali za moto zinapotokea.
0 comments:
Post a Comment